Shirika la Habari la Ahlul_Bayt (a.s) -ABNA- limeripoti kuwa, kwa mujibu wa Tovuti Rasmi ya Harakati ya Kiislamu Nigeria, Sheikh Zakzaky alihutubia mkutano huo akiwa nchini Iran kupitia mtandao. Aliwapongeza Waislamu kwa kumbukumbu tukufu ya kuzaliwa kwa Mbora wa viumbe, Mtume Mtukufu Muhammad (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na kizazi chake kitoharifu).
Akiutaja mwezi wa kuzaliwa kwa Mtume (s.a.w.w) kuwa ni kipindi cha mshikamano wa Umma wa Kiislamu, alisema:
“Maadui hawakuficha uadui wao dhidi ya Waislamu; wamesema wazi kwamba hawana maadui wengine isipokuwa Waislamu. Maadui wa Uislamu walijaribu kuangamiza nchi za Kiislamu kama Libya, ambayo waliweza kuiharibu; Sudan ambayo sasa ipo katika mzozo; pia waliangamiza Syria, Afghanistan na Iraq. Lengo lao linalofuata sasa ni Iran.”
Aidha aliongeza: “Huu ndio wakati muafaka kwa Waislamu kuungana kwa hiari yao bila kuruhusu maadui wa Uislamu kutuchochea kupingana sisi kwa sisi. Umoja ni amri ya Mwenyezi Mungu. Shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu wala msifarakiane….”
Sheikh Zakzaky alisisitiza kuwa mifarakano imeharamishwa katika Uislamu kutokana na athari zake mbaya.
Katika kipindi cha siku tano za mihadhara ya Wiki ya Umoja, wanazuoni kutoka madhehebu tofauti walitoa hotuba kuhusu mada zinazohusiana na mshikamano wa Umma wa Kiislamu.
Your Comment